Watu 3 wanaohusishwa na utekaji nyara katika kaunti 4 washtakiwa Murang'a
Watu watatu wanaoshukiwa kuhusika na visa vya utekaji nyara na wizi katika kaunti nne wamefikishwa katika mahakama ya Murang’a baada ya kukamatwa Ijumaa wiki iliyopita..
Washukiwa hao watatu Godfrey Njeru, Caroline Kairu na Caroline Mueni walifikishwa mbele ya hakimu mkuu mkaazi Erick Musambai ambapo walikana mashtaka saba yanayowakabili yakiwemo wizi, utekaji nyara na kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu. Washukiwa hao walikuwa wanasakwa katika kaunti nne za Nairobi, Murang’a, Kiambu na Nakuru kwa kuhusika na visa kadhaa vya uhalifu. Hakimu musambai aliamuru wazuiliwe kwa siku saba na wanatarajiwa tena mahakamani tarehe 20 mwezi huu. Washukiwa hao walikamatwa katika eneo la Kangema baada ya polisi kupokea habari kwamba walikuwa wamemteka nyara mwanamke mmoja na kutishia kumuua iwapo familia yake haitawalipa fedha..